Watu watano kati ya saba waliougua ugonjwa usiojulikana katika Wilaya ya Bukoba Vijijini Mkoani Kagera wamefariki dunia.
Taarifa iliyotolewa Alhamis Machi 16, 2023 na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu amesema ugonjwa huo umetokea katika vijiji vya Bulinda na Butayaibega vilivyopo katika kata za Marua Kanyangereko wilayani humo.
Profesa Nagu amesema watu hao walipata dalili za homa, kutapika, kutokwa na damu maeneo mbalimbali ya mwili na figo kushindwa kufanya kazi.
“Wengine (watu) wawili wako hospitali wanaendelea matibabu. Mwenendo wa ugonjwa huo unaashiria uwezekano kuwa ni ugonjwa wa kuambukiza,” amesema Profesa Tumaini bila kusema ni ugonjwa gani.
Amesema Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu kuhusu mwenendo wa ugonjwa huo na kuchukua hatua za kuudhibiti ili usisambae nchini.
Amezitaja hatua zinazochukuliwa ni kuchukua sampuli kwa wagonjwa na waliofariki dunia ili kubaini chanzo na kuthibitisha ugonjwa huo.
Pia amesema timu za kitaalam za kukabiliana na mlipuko katika ngazi ya mkoa na halmashauri zimetumwa kwenye maeneo yaliyoathirika na ugonjwa huo na zinaendelea na uchunguzi pamoja na hatua za udhibiti.
Ametaja hatua nyingine wanazochukua ni kufuatilia watu wenye viashiria vya ugonjwa katika jamii na vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na waliotangamana na wagonjwa hao ili kupata huduma stahiki za matibabu.
“Dawa, vifaa muhimu vipo katika vituo vya kutolea huduma za afya mkoani Kagera na wagonjwa wanaendelea na matibabu. Elimu ya afya inaendelea kutolewa kwa jamii katika mkoa wa Kagera ili kuchukua tahadhari,” amesema.
Profesa Tumaini amewataka watu kuendelea kuwa watulivu na kuchukua hatua mbalimbali wakati Serikali ikifuatilia mwenendo wa ugonjwa huo.
Amezitaja hatua hizo ni pamoja na mtu yoyote mwenye dalili za homa, kutapika, kuharisha na kutoka damu na mwili kuishiwa nguvu kuwahi katika kituo cha kutolea huduma za afya mapema kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.
“Kutoa taarifa mapema kwenye kituo cha kutolea huduma kilichoko karibu ama kupiga simu namba 199 bila malipo endapo utamuona au kukutana na mtu mwenye dalili kama hizo,” amesema.
Profesa Tumaini pia amewataka watu kuepuka kumgusa mgonjwa au majimaji ya mwili mfano mate, machozi, damu, mkojo na kinyesi yatokayo kwa mgonjwa ama mtu mwenye dalili hizo.
Amesema iwapo mtu atalazimika kumhudumia mgonjwa kwa dharura, achukue tahadhari ya kujikinga majimaji yoyote kabla ya kumhudumia.
Amewataka watu wanawe mikono kwa maji tiririka na sabuni ama kutumia vitakasa mkono ili kujikinga na magonjwa yote ya kuambukiza na kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono.
“Kushirikisha wataalam wa afya katika shughuli za misiba na mazishi katika kipindi hiki. Nawakumbusha watumishi wa afya kuzingatia kanuni za kujikinga na magonjwa ya kuambukiza (IPC) wakati wa kutoa huduma,” amesema.
No comments:
Post a Comment